Waliberia wasubiri kwa shauku kuu matokeo ya urais
Tume ya Uchaguzi nchini Liberia imewataka wananchi kuvuta subiri na kutoeneza habari za urongo zinazohusiana na matokeo ya uchaguzi wa rais.
Vyombo vya habari nchini humo vimetangaza matokeo yasio rasmi yanayoonyesha kuwa yumkini uchaguzi huo ukaingia duru ya pili, kati ya wawaniaji wawili wanaongoza kufikia sasa, ambao ni mchezaji soka nyota wa zamani wa kimataifa Seneta George Weah na Makamu wa Rais Joseph Boakai.
Mapema leo habari za tetesi katika mitandao ya kijamii zilidai kuwa tayari Geroge Weah ameibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo wa rais umevutia wagombeaji 20, wanaotaka kurithi mikoba ya Rais Ellen-Johnson Sirleaf, ambaye anaondoka madarakani baada ya kuongoza kwa mihula miwili.
Sirleaf ambaye ni rais wa kwanza mwanamke kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia nchini humo na pia mshindi wa Tuzo ya Nobel aliingia madarakani mwaka 2006, baada ya mtangulizi wake Charles Taylor, kuondolewa madarakani kwa nguvu na waasi mwaka 2003.
Waangalizi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) wamesema uchaguzi huo kwa kiasi kikubwa una itibari, ingawaje kasoro za hapa na pale zilishuhudiwa.
Hata hivyo kinara wa chama cha Liberty, Charles Brumskine ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoendelea kutangaza matokeo ya urais, vinginevyo ataichukulia hatua za kisheria. Anadai kuwa uchaguzi huo umekubwa na utata na kasoro chungu nzima.
NEC ilitazamiwa kutangaza matokea ya awali hii leo, lakini baadhi ya duru za habari ndani ya tume hiyo zimedokeza kuwa huenda matokeo hayo yakatangazwa kesho Ijumaa.