Mmarekani aliyemtukana Rais Mugabe wa Zimbabwe aswekwa jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36138-mmarekani_aliyemtukana_rais_mugabe_wa_zimbabwe_aswekwa_jela
Polisi nchini Zimbabwe imemtia mbaroni raia wa Marekani kwa tuhuma za kumtusi Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2017 10:54 UTC
  • Mmarekani aliyemtukana Rais Mugabe wa Zimbabwe aswekwa jela

Polisi nchini Zimbabwe imemtia mbaroni raia wa Marekani kwa tuhuma za kumtusi Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo.

Martha O‘Donovan, ambaye anafanya kazi katika shirika la Magamba TV amekamatwa leo Ijumaa huku polisi wakichukua kipakatalishi chake kwa madai kuwa amemvunjia heshima kiongozi wa taifa.

O'Donovan anadaiwa kuandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa Rais Mugabe ni shetani, ingawaje kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Chama cha Mawakili wa Kutetea Haki za Binadamu nchini humo kimesema maafisa polisi mapema leo wamevamia makazi ya raia huyo wa Marekani mjini Harare na kumtia nguvuni.

Kadhalika vyombo vya usalama vimefunga akaunti ya Twitter ya Martha O‘Donovan.

Mugabe na mkewe Joyce (Kulia)

Kanali ya Televisheni ya Magamba imekuwa ikitengeza filamu fupi za kisiasa zinazokejeli na kuikosoa serikali.

Ubalozi wa Marekani mjini Harare umethibitisha kuwa Mmarekani huyo amekamatwa na kwamba unafuatilia kwa karibu kesi hiyo.

Iwapo raia huyo wa Marekani atapatikana na hatia, huenda akahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.