Rais wa Zambia awaonya majaji wasifuate mkondo wa wenzao wa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36140-rais_wa_zambia_awaonya_majaji_wasifuate_mkondo_wa_wenzao_wa_kenya
Rais Edgar Lungu wa Zambia ametoa tahadhari kwa majaji wa nchi hiyo dhidi ya kufuata mkondo wa majaji wa Kenya wa kumzuia kugombea urais katika uchaguzi ujao nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 03, 2017 11:01 UTC
  • Rais wa Zambia awaonya majaji wasifuate mkondo wa wenzao wa Kenya

Rais Edgar Lungu wa Zambia ametoa tahadhari kwa majaji wa nchi hiyo dhidi ya kufuata mkondo wa majaji wa Kenya wa kumzuia kugombea urais katika uchaguzi ujao nchini humo.

Lungu aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mkutano wa hadhara mjini Solwezi, kaskazini magharibi mwa nchi akihutubia wafuasi wake ambapo alisisitiza kuwa: "Msiwe watu wa kuiga, kisha mudhani mtaonekana mabingwa iwapo mtaitumbukiza nchi hii katika machafuko. Najua watu ambao hawaipendei amani na uhuru nchi hii watadai kuwa Rais Lungu anatishia vyombo vya mahakama. Mimi sitishii mahakama, bali nawapa tu indhari wale wanaotaka kulisukuma taifa katika ghasia."

Vyama vya upinzani tayari vimekosoa vikali azma ya Lungu ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2021 kwa muhula wa tatu, kwani kisheria, hafai kuwania urais kwa zaidi ya vipindi viwili.

Majaji wa Mahakama ya Juu ya Kenya

Itakumbukwa kuwa, Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8 na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike ndani ya siku 60, hatua ambayo iliibua gumzo la kisiasa ndani na nje ya nchi.

Serikali ya Zambia imekuwa ikikosolewa kwa kuwawekea mbinyo viongozi wa upinzani na wakosoaji wake.

Hakainde Hichilema ambaye ni mkuu wa chama cha upinzani cha UPND alikamatwa na vyombo vya usalama nchini humo mwezi Aprili mwaka huu, kwa tuhuma za kupanga njama ya kuipindua serikali na kisha akaachiwa huru mwezi Agosti.