Wanamgambo kumi wa kundi la al Shabab wauawa Somalia
Wanamgambo wasiopungua kumi wa kundi la al Shahab wameuawa katika mapigano kati yao na vikosi vya usalama vya Somalia.
Ahmad Musa Nur Naibu Gavana wa mkoa wa Mudug katikati mwa Somalia ameeleza kuwa wanamgambo hao wa al Shabab wameuawa katika kijiji kimoja cha pwani ya eneo la kistratejia huko kaskazini mashariki mwa Somalia kwenye mapigano yaliyojiri kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo hao; na wakati huo huo vikosi vya usalama vya Somalia vimemtia mbaroni mwanamgambo mwingine wa kundi hilo.
Hii ni katika hali ambayo Radio ya Shabelle ya Somalia leo imetangaza kuwa idadi ya kadhaa ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo pia vimeuawa katika mapigano hayo na wanamgambo wa al Shabab. Vikosi vya serikali ya Somalia katika miezi kadhaa iliyopita vilizidisha oparesheni zake dhidi ya wanamgambo wa al Shabab katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita pia wanamgambo wa al Shabab waliishambulia karakana ya makaa ya mawe katika eneo karibu na mji wa pwani wa Kismayo na kuwauwa wafanyakazi watatu na kujeruhi wengine sita.