Nov 30, 2017 16:32 UTC
  • Kenya na Tanzania zaelekea katika mzozo wa maji

Ukanda wa Hifadhi za Taifa za Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara nchini Kenya ambao una mojawapo wa maajabu manane ya dunia yanayovutia watalii unakumbwa na tishio la kimazingira kutokana na nchi hizo mbili kuingia katika mgogoro wa kugombania maji.

Mgogoro huo unatokana na uamuzi wa Serikali ya Kenya kujenga mabwawa mawili katika Mto Mara ambayo wataalamu wanaonya kuwa, yatakausha ukanda huo na kuathiri uzao wa ndege katika Ziwa Natron huku Tanzania ikipanga kuwa maji katika mto huo hayatatiririka ipasavyo katika Ziwa Victoria.

Kenya inatarajia kuwa, mradi huu utasaidia kumwagilia mashamba karibu na chanzo cha mto huo katika Msitu wa Mau na kumaliza tatizo la maji kwa wakazi wa maeneo hayo.

Hata hivyo wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa, hatua hiyo itaathiri zaidi upatikanaji wa maji ukanda mzima hasa mwisho wa mto huo na madhara hayo kuathiri hadi Tanzania. 

Mbuga ya wanyama ya Serengeti, Tanzania

 

Mto Mara ni maarufu duniani kutokana na wanyama wengi, hasa nyumbu, kuuvuka kila mwaka kutoka upande mmoja hadi mwingine.

Kitendo cha wanyama hao kuhama kila mwaka kwa kujikusanya pamoja na kujitupa kwenye mto wenye mamba lukuki ili kuvukia upande wa pili kimelifanya tukio hilo kuwa moja ya maajabu manane duniani. 

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania

Inakadiriwa kuwa idadi ya nyumbu takriban 1.5 milioni wakisindikizwa na kundi kubwa la pundamilia, pofu, swala na digidigi huhama kila mwaka kutoka Serengeti nchini Tanzania na kwenda Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya katika jitihada za kutafuta chakula.

Tags