Mkuu wa Wakristo wa Misri akataa kuonana na Naibu wa Trump
Mkuu wa Wakristo wa Qibti nchini Misri amekataa kuonana na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, kutokana na Donald Trump kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa Israel.
Kanisa la Wakristo wa Qibti nchini Misri limetoa taarifa na kusema kuwa, Papa Tawadros II, kiongozi wa Wakristo hao amekataa kuonana na naibu wa Donald Trump ambaye ilikuwa aonane naye mwishoni mwa mwezi huu mjini Cairo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Papa Tawadros II amekataa kuonana na Mike Pence kutokana na Trump kutangaza kuwa Quds ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kabla ya hapo Sheikh al Azhar Ahmed el-Tayeb alilaani uamuzi huo wa Donald Trump na kusema kuwa ni kinyume cha sheria na kuwataka maulamaa wa Kiislamu kuitisha kikao cha dharura cha kuzungumzia njia za kuchukua kukabiliana na uadui huo mpya wa rais wa Marekani.
Uamuzi huo wa rais wa Marekani unaendelea kulaaniwa katika kila kona ya dunia huku kwenye baadhi ya maeneo kukiwa kunafanyika maandamano ya kila siku kulaani jaribio la Marekani la kuwapokonya Waislamu Kibla chao cha Kwanza yaani Masjidul Aqswa kupitia kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala ghasibu wa Kizayuni.