ICC kuishitaki Jordan kwa kukataa kumtia nguvuni Rais wa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37487-icc_kuishitaki_jordan_kwa_kukataa_kumtia_nguvuni_rais_wa_sudan
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa itairipoti Jordan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kukataa kumtia nguvuni Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipokuwa safari nchini humo mwezi Machi mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 11, 2017 23:06 UTC
  • ICC kuishitaki Jordan kwa kukataa kumtia nguvuni Rais wa Sudan

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetangaza kuwa itairipoti Jordan katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na kukataa kumtia nguvuni Rais Omar al-Bashir wa Sudan alipokuwa safari nchini humo mwezi Machi mwaka huu.

Rais wa Sudan alikuwa Aman mji mkuu wa Jordan tarehe 29 mwezi Machi ambako alihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).

Wakati huo jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu kama Human Rights Watch (HRW) ziliitaka Jordan kumtia nguvuni Rais Omar al Bashir wa Sudan kwa tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita katika eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.

Mwaka 2009 na 2010 pia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa waranti wa kutiwa nguvuni kiongozi huyo wa Sudan kwa tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari huko Darfur na kuzitaka nchi zote wanachama kutekeleza agizo hilo.

Maelfu ya raia wameuawa Darfur, Sudan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina mamlaka ya kuiwekea vikwazo nchi yoyote mwanachama inayokataa kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mauaji na machafuko yanayoendelea katika jimbo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.