Rais wa Msumbiji awapiga kalamu nyekundu mawaziri wanne
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37553-rais_wa_msumbiji_awapiga_kalamu_nyekundu_mawaziri_wanne
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amewafuta kazi mawaziri wanne wakiwemo wa mambo ya nje na mafuta. Hata hivyo ofisi yake haijatoa sababu ya kupigwa kalamu nyekundu mawaziri hao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2017 11:48 UTC
  • Rais wa Msumbiji awapiga kalamu nyekundu mawaziri wanne

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amewafuta kazi mawaziri wanne wakiwemo wa mambo ya nje na mafuta. Hata hivyo ofisi yake haijatoa sababu ya kupigwa kalamu nyekundu mawaziri hao.

Taarifa ya Ikulu ya Rais imesema Ernesto Max Elias Tonela ameteuliwa kuchukua nafasi ya Leticia da Silva Klemens kama Waziri wa Nishati na Madini, huku Jose Condugua Antonio Pacheco akiteuliwa kurithi mikoba ya Waziri wa Mambo ya Nje, Oldemiro Baloi.

Kadhalika Rais wa Msumbiji katika mabadiliko hayo madogo amewafuta kazi mawaziri wa viwanda na biashara, kilimo na usalama wa chakula.

Licha ya utajiri wa maliasili, wananchi wengi wa Msumbiji wanasumbuliwa na hali ngumu ya maisha

Hii sio mara ya kwanza kwa rais huyo kuwatimua kazi maafisa wa ngazi za juu pasina kutoa sababu yoyote.

Mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, kiongozi huyo aliwafuta kazi Mkuu wa Shirika la Upelelezi, Lagos Lidimo na Graça Chongo, na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo wiki mbili baada ya mauaji ya watu 16 katika shambulizi lililofanyika kaskazini mwa nchi hiyo.

Hata hivyo taarifa ya Rais wa Msumbiji haikutaja sababu ya kufutwa kazi maafisa hao wa juu wa masuala ya upelelezi na jeshi.