George Weah ashinda urais Liberia, amshukuru Arsene Wenger, Jacob Zuma ampongeza
Bingwa wa zamani wa dunia wa mpira wa miguu, George Weah ameshinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa nchi ya magharibi mwa Afrika ya Liberia kwa kukomba kaunti 12 kati ya 15 za nchi hiyo zilizopiga kura.
George Weah ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa timu ya AC Milan ya Italia amechaguliwa kuwa rais wa 25 wa Liberia. Katika duru hiyo ya pili amemshinda kwa mbali mpinzani wake, Joseph Boakai aliyepata kaunti mbili tu kati ya 15 za nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa Boakai alikuwa makamu wa rais wa Liberia kwa muda wa miaka 12.
Weah aliwahi pia kuzichezea timu za Chelsea na Manchester City za Uingereza na amewahi kuwa mchezaji bora wa Afrika mara tatu.
Rais huyo mteule wa Liberia anamshukuru sana kocha wa timu ya Arsenal ya Uingereza kwa kusema: Arsene Wenger alikuwa kama baba yangu na mimi nilikuwa kama mwanawe. Mtu huyo alinionesha mapenzi katika wakati ambao ubaguzi wa rangi ulikuwa umechachamaa. Alinitaka niingie uwanjani nicheze kwa ajili yake yeye tu kila siku.
Huku hayo yakiripotiwa, rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ametuma pongeza zake kwa George Weah kwa ushindi aliopata katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyofanyika Liberia tarehe 26 mwezi huu wa Disemba 2017.

Katika taarifa yake aliyoitoa leo, Rais Jacob Zuma ameipongeza Liberia kwa kuendesha uchaguzi katika mazingira ya utulivu na kusema kuwa, hilo limeonesha mfano mwingine mzuri unaotia nguvu kusimamishwa demokrasia ya kweli barani Afrika.
Weah atachukua nafasi ya Rais Ellen Johnson-Sirleaf (79) ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika kuwa rais wa nchi na amirijeshi mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi.