Naigeria yamsaili balozi wa Marekani, baada ya Trump kuwatukana Waafrika
Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imemwita na kumsaili balozi wa Marekani mjini Abuja ikiwa ni katika kupinga matamshi ya kejeli na matusi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Afrika na Waafrika.
Hatua hiyo ya Nigeria inafuatia ile ya nchi kadhaa za bara la Afrika kama Senegal, Afrika Kusini na Botswana ambazo zimewaita na kuwasaili mabalozi wa Marekani baada ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump kuzitusi nchi za Afrika kwamba ni shimo la kinyesi!
Vilevile Umoja wa Afrika umelaani vikali matusi na kejeli hizo za Trump na kusema kuwa, Rais wa Marekani anapaswa kuwaomba radhi Waafrika baada ya kuwatusi na kuwavunjia heshima.
Ebba Kalondo, msemaji wa Moussa Faki Mahamat, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema kuwa, matamshi hayo ya Trump katu hayakubaliki na yamewavunjia heshima Waafrika.
Sehemu moja ya taarifa ya Umoja wa Afrika imesema: Matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu bara Afrika yanaonyesha ubaguzi wa wazi alionao Rais huyo.
Nchini Tanzania pia, mkuu wa chama za ACT Wazalendo, Zito Zuberi Kabwe alitaka rais huyo wa Marekani, Donald Trump achukuliwe hatua kali.
Jumapili iliyopita pia wananchi wa Kenya waliungana na Waafrika wenzao na wapenda haki duniani kulaani matusi hayo ya Rais wa Marekani, Donald Trump.
Matamshi hayo ya Trump yamelaaniwa pia ndani ya Marekani kwenyewe ambako Spika wa Kongresi, Paul Ryan ameyataja kuwa ni ya kibaguzi.