UN: Watu laki moja wanahitajia msaada Jamhuri ya Afrika ya Kati
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema takriban watu laki moja wanahitajia msaada katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Stephane Dujarric amesema wakazi wa mji wa Paoua wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na mapigano ya kila kuchao kati ya magenge ya wabeba silaha.
Amesema wakazi elfu 60 wa mji huo wamekimbilia mji jirani ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Chad kutokana na makabiliano hayo, huku wengine wapatao 40 elfu wakilazimika kuwa wakimbizi wa ndani.
Dujarric amesema iwapo mapigano hayo yataendelea, basi idadi ya wakimbizi wa ndani katika mji huo itaongezeka maradufu au mara tatu. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema aghalabu ya wakimbizi hao ni watoto wadogo na wanawake.
Ameongeza kuwa, hali ya kiafya katika mji huo inatisha, huku kukiweko na madai kuwa maiti za watu waliouawa katika mapigano hayo zimetupwa kwenye visima na baadhi zimetapakaa vijijini.