Chama cha Umma chawataka wananchi kuandamana dhidi ya serikali ya Sudan
Chama cha Umma cha nchini Sudan kimewatolea mwito wananchi kuandamana dhidi ya serikali ya Khartoum.
Maandamano hayo yamepangwa kufanyika siku ya Jumatano tarehe 31 mwezi huu katika maidani ya al Sha'bey huko Khartom mji mkuu wa Sudan. Katika taarifa iliyotolewa na chama cha Umma cha nchini Sudan kunaonekana kaulimbiu kama vile "wakabidhi wananchi madaraka ya nchi," "Umechafua sura ya Uislamu" na "Ondoka Ondoka!"
Hivi karibuni vyombo vya kuaminika nchini Sudan viliripoti habari ya kutiwa mbaroni waandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa na Reuters nchini humo ambao walikuwa wakiandaa ripoti kuhusu maandamano hayo dhidi ya serikali huko Khartoum.
Maandamano yalianza huko Sudan tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari baada ya serikali kuanza kuchukua hatua kali za kiuchumi na za kubana matumizi katika kutekeleza siasa za Mfuko wa Fedha Duniani (IMF).