Odinga 'aapishwa' kuwa 'rais wa wananchi' Kenya, viongozi wenzake wasusa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39693-odinga_'aapishwa'_kuwa_'rais_wa_wananchi'_kenya_viongozi_wenzake_wasusa
Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga 'ameapishwa' hii leo kuwa 'rais wa wananchi' katika sherehe ilizofanyika katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 30, 2018 13:21 UTC
  • Odinga 'aapishwa' kuwa 'rais wa wananchi' Kenya, viongozi wenzake wasusa

Kinara wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga 'ameapishwa' hii leo kuwa 'rais wa wananchi' katika sherehe ilizofanyika katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi.

Hata hivyo sherehe hiyo imekosa msisimko wa aina yake, kwa kutohudhuriwa na vinara wengine wa muungano wa NASA, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.

Odinga ameapishwa licha ya Mwanasheria Mkuu nchini humo, Profesa Githu Muigai kumuonya kuwa hatua hiyo inakiuka katiba na huenda atafunguliwa mashtaka ya uhaini.

Baada ya kula kiapo hicho chenye utata kilichoongozwa na Mbunge wa Ruaraka jijini Nairobi, TJ Kajwang, Odinga ameuambia umati mkubwa ulijitokeza kwenye uwanja huo kuwa, “Kalonzo, Mudavadi na Wetangula hawapo hapa, lakini wako pamoja nasi, mtafahamishwa ni kwanini hawakufika.” 

Odinga na vinara wenza wa NASA

Odinga anasisitiza kuwa alishinda uchaguzi uliofanyika Agosti 8 mwaka uliopita, uchaguzi ambao ulibatilishwa na mahakama iliyaomuru uchaguzi wa marudio ufanyike. Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alitangazwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 26 ambao Odinga aliusisia.

Hii ni katika hali ambayo, Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo imezima radio na televisheni za Kenya ambazo zimekuwa zikirusha matangazo ya moja kwa moja ya NASA katika uwanja wa Uhuru Park.

Wakati huo huo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Mating'i ameliorodhesha vuguvugu la NRM ambalo liko chini ya NASA kuwa kundi la kigaidi kama vile al-Shabaab na Mungiki.

Kinachosuburiwa kwa sasa ni kuona hatua atakayochukua kiongozi huyo wa upinzani baada ya kula kiapo cha kuwa rais wa wananchi, licha ya kuwa Kenya ina Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.