Maandamano dhidi ya Israel yaendelea nchini Tunisia
Mamia ya wanaharakati wa kisiasa na kijamii wa nchini Tunisia kwa mara nyingine wamefanya maandamano wakilitaka bunge la nchi hiyo lifanye haraka kupitisha sheria ambayo itatamka wazi kuwa ni uhalifu kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel
Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa, mamia ya wananchi wa Tunisia leo Jumatatu wameendelea na maandamano yao kwa siku ya pili mfululizo wakilishinikiza bunge lipasishe haraka sheria itakayopiga marufuku kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waandamanaji hao wamelitaka bunge lifanye haraka kupasisha muswada uliopendekezwa na vyama vya siasa mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana ambao kama utapasishwa na kuwa sheria, basi suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel litakuwa ni uhalifu nchini humo.
Waandamanaji wamebeba bendera za Palestina na mabango yenye maandishi ya kuilaani vikali Israel na kuliunga mkono taifa linalodhulumiwa la Palestina.
Vile vile waandamanaji hao wametishia kuwa, iwapo bunge la Tunisia litaendelea kupuuza jambo hilo, basi maandamano ya wananchi yatakuwa makubwa na makali zaidi.
Mrengo wa wananchi wa Tunisia unaoundwa na vyama kadhaa, tarehe 31 Disemba 2017 uliwasilisha muswada bungeni wa kutaka suala la kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel lihesabiwe kuwa ni uhalifu nchini humo. Hata hivyo bunge la Tunisia linaonekana kupuuza suala hilo kiasi kwamba kamati ya sheria na uhuru mbalimbali ya bunge hilo, wiki iliyopita iliakhirisha mjadala kuhusiana na jambo hilo.