Imarati inatumia pesa zilizozuiwa za Libya kuwaunga mkono wapiganaji wa Haftar
Makamu wa pili wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Libya amesema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) unatumia pesa zilizozuiwa za Libya kuwaunga mkono wapiganaji wa kamanda wa jeshi la taifa la nchi hiyo.
Mohammad Am'azb Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Libya huku akitegemea taarifa zilizotolewa ametangaza kuwa Imarati imetwaa na kutumia pesa za Libya zilizozuiwa katika mabenki ya Imarati kwa ajili ya kusaidia oparesheni za wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya mashariki mwa nchi hiyo.
Mohammad Am'azb ameongeza kuwa gharama za fedha za kituo cha jeshi la anga cha al Khadim huko mashariki mwa mji wa Benghazi Libya zinatokana na fedha hizo zilizozuiwa huko Imarati.
Makamu wa Pili wa Mwenyekiti wa Baraza Kuu la serikali ya Libya pia ameitaka Imarati itangaze wazi vyanzo vya kifedha wanavyotumia kuwaunga mkono wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftari ili ikadhibishe kama kweli haijatwaa fedha hizo za Libya zilizozuiliwa. Umoja wa Mataifa mwaka 2011 ulichukua uamuzi wa kuzuia mali za Libya katika benki zote duniani ili kuzuia kuibiwa fedha za nchi hiyo na Muammar Gaddafi dikteta wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani. Kiwango cha pesa za Libya zilizozuiwa katika nchi kadhaa za Magharibi zinafikia makumi ya mabilioni ya dola.