Somalia yaitaka UN kusitisha uvamizi wa Imarati Somaliland
Mwakilishi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa amelaani hatua ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ya kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ametaka hatua za lazima zichukuliwe ili kusitisha uchokozi huo wa Imarati.
Abukar Dahir Osman amesema kuwa mwaka jana Imarati ilitiliana saini makubaliano na maafisa wa eneo lenye utawala wa ndani la Somaliland kuhusu kuanzisha kituo cha kijeshi cha Imarati katika bandari ya Berbera.
Osman ameongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya wataalamu wa kamati maalumu ya vikwazo kwa Somalia na Eritrea, kitendo cha kujenga kituo hicho na kupeleka zana za kijeshi katika eneo hilo ni kukiuka azimio linalohusiana na vikwazo vya silaha vya Somalia.
Mwakilishi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa hatua zinazochukuliwa na Imarati nchini Somalia ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kwa hiyo serikali ya Somalia inaliomba Baraza la Usalama lichukue hatua za lazima za kuilazimisha Abu Dhabi ikomeshe uchokozi wake huo.
Wakati huo huo Ahmed Isse Awad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia ameyataja makubaliano hayo kati ya Imarati na eneo la Somaliland kuwa ni kinyume cha sheria na ni uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na ardhi nzima ya Somalia.