Chama cha Umma Sudan chakadhibisha madai ya serikali
Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan, National Umma Party (NUP) kimetangaza kuwa hatua zinaochukuliwa na serikali ya Khartoum dhidi ya kiongozi wa chama hicho, Sadiq al Mahdi ni hatari sana na zinatishia amani na usalama wa nchi hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Fadlallah Burma Nasser amesema tuhuma zilizotolewa na serikali ya Sudan dhidi ya Sadiq al Mahdi ni za kubuniwa na za uongo. Amesema kuwa chama hicho kimetiliana saini na harakati za waasi waraka wa kusitisha machafuko na kutafuta suluhisho na matatizo yaliyopo na si kwa ajili ya kuvuruga amani, kutumia mabavu na kuoindoa madarakani serikali, kama wanavyodai watawala wa Khartoum.
Matamshi hayo yametolewa baada ya Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Sudan kutoa tuhuma kadhaa dhidi ya Sadiq al Mahdi ambazo hukumu yake ni kifo. Kiongozi huyo wa chama cha upinzani cha Umma anakabiliwa na tuhuma za ugaidi na kushirikiana na makundi ya waasi dhidi ya serikali ya Rais Omar al Bashir.
Mwendesha Mashtaka wa serikali ya Sudan anasema: Tuhuma hizo zimetolewa baada ya Sadiq al Mahdi kutia saini waraka uliojumuisha makundi kadhaa ya waasi unaosisitiza udharura wa kushirikiana kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali ya Khartoum kwa kutumia silaha, kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kuandamana dhidi ya serikali na kuzusha machafuko na fujo.
Siku chache zilizopita pia Rais Omar al Bashir wa Sudan alitangaza bungeni kwamba, atachukua hatua za kisheria dhidi ya wanasiasa wanaoungana na kushirikiana na makundi ya waasi.