Rais Bashir wa Sudan aamuru wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i42948-rais_bashir_wa_sudan_aamuru_wafungwa_wote_wa_kisiasa_waachiliwe_huru
Rais Omar al Bashir wa Sudan ametoa amri ya kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2018 03:00 UTC
  • Rais Bashir wa Sudan aamuru wafungwa wote wa kisiasa waachiliwe huru

Rais Omar al Bashir wa Sudan ametoa amri ya kuachiliwa huru wafungwa wote wa kisiasa nchini humo.

Bashir ametoa amri hiyo wiki kadhaa baada ya idadi kubwa ya wanaharakati wa upinzani kukamatwa wakati wa maandamano makubwa dhidi ya serikali. Maandamano hayo yalikuwa yameitishwa kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi hasa ughali wa mkate katika nchi hiyo ambapo baadhi ya wapinzani pia walitaka serikali ya Bashir ipinduliwe.

Shirika rasmi la habari la Sudan, Suna, limesema uamuzi huo wa Bashir unalenga kuleta amani na maelewano kwa ajili ya kuandaa mazingira mazuri ya kufikiwa malengo ya kitaifa. Taarifa hiyo haikusema ni wafungwa wangapi wa kisiasa walio katika korokoro za nchi hiyo wala haikutaja majina yao.

Wanaharakati wa upinzani wanasema kuna wafungwa 50 wa kisiasa akiwemo mwanasiasa mashuhuri, Mohammad Mukhtar al Khatib ambaye ni kiongozi wa chama cha kikomunisti.

Hivi karibuni chama tawala cha National Congress (NCP) kilisema kuna mpango wa kufanya mazungumzo ya kitaifa ili kuitafutia suluhiso la kudumu migogoro ya kisiasa nchini humo.