Uhusiano wa Somalia na Umoja wa Falme za Kiarabu wazidi kuzorota
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43148-uhusiano_wa_somalia_na_umoja_wa_falme_za_kiarabu_wazidi_kuzorota
Mzozo katika uhusiano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Somalia umezidi kuzorota kutokana na hatua ya Imarati kuingilia mambo ya ndano ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2018 12:13 UTC
  • Uhusiano wa Somalia na Umoja wa Falme za Kiarabu wazidi kuzorota

Mzozo katika uhusiano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Somalia umezidi kuzorota kutokana na hatua ya Imarati kuingilia mambo ya ndano ya nchi hiyo.

Katika tukio la hivi karibuni, ndege moja ya  maafisa wa kijeshi wa Imarati ilishikiliwa kwa masaa kadha katika Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa Bosaso katika eneo la Puntland lenye mamlaka ya ndani baada ya maafisa hao wa Imarati kukataa mizigo yao ikaguliwe.

Ukaidi huo wa Waimarati ulipelekea kuwepo na msuguano ulioendelea kwa masaa kadhaa baada ya wakuu wa Somalia kusisitiza kuwa lazima mizigo hiyo ikaguliwe. Taarifa zinasema hatimaye, Waimarati waliafiki mizigo yao ikaguliwe na kisha wakaruhusiwa kupita.

Tukio hilo ni sawa na lile la hivi karibuni ambapo meli moja yenye bendera ya Imarati ilikatazwa kutia nanga katika bandari ya Bosaso.  Wiki iliyopita, Serikali ya Kifiderali ya Somalia ilinasa dola milioni 9.6 ambazo zilikuwa katika mifuko iliyokuwa katika ndege ya UAE Royal iliyotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu.

Somalia ililalamika kuwa fedha hizo zilikuwa zinalenga kutumiwa kuibua fitina katika nchi hiyo. Uhusiano wa UAE na Somalia ulianza kuzorota pale nchi hiyo ya Kiarabu ilivyoanza kuunga mkono wazi wazi eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland. Pasina kupata idhini ya serikali ya Mogadishu, Imarati ilianza kujenga kituo chake cha kijeshi katika eneo hilo sambamba na kuanza kutumia bandari ya eneo hilo bila idhini kitendo ambacho wakuu wa Mogadishu wanasema ni dharau ya wazi. Hivi sasa serikali ya Somali inasema inapanga kuwasilisha malalamiko rasmi katika vyombo vya kimatiafa dhidi ya Imarati kutokana na hatua yake ya kujenga kituo chake che kijeshi katika eneo hilo la Somaliland.