Serikali ya Somalia yapinga kuingiliwa katika masuala yake ya ndani
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia amesema kuwa, serikali na wananchi wa nchi hiyo wanapinga uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo
Mtandao wa Habari wa al-A'had umemnukuu Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia akitangaza kuwa, Bunge la nchi hiyo limepasisha kwa wingi wa kura kupiga marufuku kunufaika Shirika la Bandari la Dubai na bandari za Somalia na kufuta mikataba yote iliyotiwa saini baina ya bandari za nchi mbili hizo.
Serikali ya Somalia inalituhumu Shirika la Bandari la Dubai kwamba, limekuwa likiendesha harakati za kutiliwa shaka, limekuwa likikiuka wazi mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo pamoja na kutishia umoja wa nchi hiyo ya Pembe yya Afrika.
Mzozo katika uhusiano baina ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Somalia umezidi kuzorota kutokana na hatua ya Imarati ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Kiafrika.
Wiki iliyopita, Serikali ya Kifiderali ya Somalia ilinasa dola milioni 9.6 ambazo zilikuwa katika mifuko iliyokuwa katika ndege ya UAE Royal iliyotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu.
Somalia ililalamika kuwa fedha hizo zilikuwa zinalenga kutumiwa kuibua fitina katika nchi hiyo. Uhusiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Somalia ulianza kuzorota pale nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi ilipoanza kuliunga mkono wazi wazi eneo lililojitenga na kujitangazia uhuru la Somaliland.