Wabunge wa Sudan wataka wanajeshi wa nchi hiyo waondoke Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43888-wabunge_wa_sudan_wataka_wanajeshi_wa_nchi_hiyo_waondoke_yemen
Wabunge nchini Sudan wamemtaka rais wa nchi hiyo Omar al Bashir achukue hatua za haraka kuondoa wanajeshi wa nchi hiyo walioko katika muungano wa kijeshi wa Saudia ambao unatekeleza hujuma dhidi ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 01, 2018 02:58 UTC
  • Wabunge wa Sudan wataka wanajeshi wa nchi hiyo waondoke Yemen

Wabunge nchini Sudan wamemtaka rais wa nchi hiyo Omar al Bashir achukue hatua za haraka kuondoa wanajeshi wa nchi hiyo walioko katika muungano wa kijeshi wa Saudia ambao unatekeleza hujuma dhidi ya Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa, wabunge wa Muungano wa 'At-Taghyir' katika Bunge la Sudan unaojumuisha wabunge huru wametoa taarifa na kusema: "Kushiriki Sudan katika vita vya Yemen ni kinyume cha katiba ya nchi."

Taarifa hiyo imesema bunge la nchi hiyo halikuafiki kutuma wanajeshi wake nchini Yemen.

Aidha wabunge hao wamesema kuwa Sudan inapaswa kujitahidi kuunga mkono jitihada za amani Yemen pasina kuunga mkono upande wowote sambamba na kuwaheshimu Wayemen pasina kuingilia mambo ya ndani ya nchi yao.

Hadi sasa pia wanasiasa wengi nchini Sudan wamemtaka Rais Omar el Bashir aondoe wanajeshi wa nchi hiyo walio katika muungano wa Saudia dhidi ya Yemen.

Watoto ni waathirika wa jinai za Saudia Yemen

Ikumbukwe kuwa mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha vita vikubwa vya kivamizi dhidi ya nchi masikini ya Kiarabu ya Yemen kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu kama vile Imarati na Sudan.

Hadi sasa Wayemen zaidi ya elfu 14,000 wameuawa huku malaki ya wengine wakijeruhiwa katika hujuma hiyo ya Yemen. Aidha mamilioni ya Wayemen wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na vita hivyo hivyo vya Saudia.

Wakati walipoanzisha uvamizi, wavamizi hao wa Yemen walikuwa na ndoto ya kumaliza vita hivyo katika muda mfupi sana, hata hivyo uvamizi huo umeingia katika mwaka wake wa nne hivi sasa na bado Saudia imeshindwa kufikia malengo yake, na ndio maana inamalizia hasira zake kwa kushambulia maeneo ya raia baada ya kuona jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimezidi kuwa na nguvu na vinaendelea kuyapiga kwa makombora maeneo ya Saudi Arabia, ukiwemo mji mkuu wake Riyadh.