Sudan kufunga balozi zake 13 nje ya nchi
Rais Omar al Bashir wa Sudan ameagiza kuandaliwa upya muundo wa kitaasisi wa mabalozi wanaoiwakilisha nchi hiyo nje ya nchi na kufungwa balozi 13 za nchi hiyo kutokana na nchi hiyo kukabiliwa na mgogoro wa fedha.
Rais wa Sudan amechukua uamuzi huo ili kupunguza gharama za matumizi kwa kuzingatia hali ya kiuchumi na kuzidisha utendaji katika Wizara ya Mambo ya Nje. Balozi 13 za uwakilishi wa kisiasa za Sudan nje ya nchi zitafungwa kwa mujibu wa agizo hilo la Rais Omar al Bashir; ambapo imeelezwa kuwa kutakuwepo na balozi mmoja tu katika jumla ya balozi saba huku balozi ndogo nne zikifungwa. Wakati huo huo wanadiplomasia wa Sudan nje ya nchi pia watakuwa wakifanya kazi kwa muda wa miaka mitatu.
Katika upande mwingine, Rais wa Sudan ameagiza kufutwa wadhifa wa mwambata wa kiuchumi na kibishara na kwamba ofisi zote za Sudan zinazohusika na masuala hayo zitafungwa isipokuwa ile ya mwambata wa kiuchumi na kibiashara iliyoko Abu-Dhabi nchini Imarati. Viongozi wa Sudan hawajaaashiria majina ya nchi ambako balozi na balozi ndogo za nchi hiyo zitafungwa. Ibrahim Ghandour Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan ambaye wiki mbili zilizopita aliuzuliwa wadhifa huo alieleza kuwa serikali haijalipa mishahara ya wanadiplomasia na mabalozi wake tangu miezi saba iliyopita.