Sudan: Mpango wa kukusanya silaha utaendelea kutekelezwa
Serikali ya Sudan imetangaza kuwa, mpango wa kukusanya silaha kama moja ya njia za kurejesha amani na uthabiti wa nchi hiyo utaendelea kutekelezwa.
Makamu wa Rais wa Sudan amesema kuwa, mpango huo utaendelea kutekelezwa hadi pale amani na uthabiti utakaposhuhudiwa katika maeneo yote ya nchi hiyo ya Kiafrika.
Hassabo Mohammed Abdel Rahman ametangaza kuwa, mpango wa kukusanya silaha katika maeneo yanayokabiliwa na vita na machafuko utaendelea kutekelezwa kikamilifu na kwamba, lengo ni kuhakikisha silaha zote zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinakusanywa.
Makamu huyo wa Rais wa Sudan ameashiria hasara za kiusalama, kijamii na kiuchumi zinazosababishwa na kuzagaa silaha kinyume cha sheria nchini humo na kubainisha kwamba, yeye pamoja na wajumbe wa kamati kuu yenye jukumu la kutekeleza mpango wa ukusanyaji silaha wametembelea maeneo yenye machafuko likiwemo jimbo la Darfur ili kujionea kwa karibu natija ya utekelezwaji wa mpango huo wa usalama.
Ni mwaka mmoja sasa umepita tangu serikali ya Sudan ilipoanza kutekeleza mpango wa ukusanyaji silaha haramu katika maeneo yenye machafuko yakiwemo majimbo ya Darfur na Kordofan Kusini lengo likiwa ni kurejesha amani na uthabiti katika maeneo hayo.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulipongeza mpango wa serikali ya Sudan wa kukusanya silaha ukisema kuwa, mpango huo umeleta amani na utulivu hususan katika jimbo la Darfur lililoko magharibi mwa nchi hiyo.