Ripoti: Saudia inafanya mipango ya kumrejesha madarakani dikteta wa zamani wa Tunisia
Chombo kimoja cha habari nchini Tunisia kimefichua kuwa Saudi Arabia inafanya njama za kumrejesha madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo.
Mtandao wa habari wa Rai Tunis umefichua kuwa: Saudi Arabia inafanya kila iwezalo kumrejesha madarakani dikteta wa zamani wa Tunisia, Zainul Abidin bin Ali aliyepewa hifadhi nchini humo.
Mtandao huo umeripoti kuwa, kufutwa kazi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia, Lutfi Braham anayetambulika kuwa mtu wa karibu kwa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, kunafungamana na mpango wa Saudia wa kutaka kumrejesha madarakani Zainul Abidin.
Tarehe 25 mwezi Februari Lutfi Braham alifanya safari ya kutatanisha nchini Saudi Arabia ambako alikutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa masuala ya kisiasa na kijasusi wa nchi hiyo.
Viongozi wa Tunisia wamekuwa wakiitaka Saudia imkabidhi dikteta huyo aliyekimbilia nchini humo baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Zainul Abidin bin Ali aliitawala Tunisia kwa kipindi cha miaka 24.