Ethiopia: Imarati, Marekani hazikuwa na nafasi katika makubaliano ya amani na Eritrea
Ethiopia imekanusha madai kwamba Imarati imekuwa na nafasi katika makubaliano ya amani iliyofikia na nchi jirani ya Eritrea.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia, Mils Alam amejibu baadhi ya taarifa kwamba Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa na mchango katika makubaliano ya amani kati ya Ethiopia na Eritrea na kusisitiza kwamba, makubaliano hayo yamesainiwa kwa hamu ya nchi mbili hizo na bila ya kutegemea upande wa tatu.
Kabla ya hapo Sultan bin Khalifa Al Nahyan, Mshauri wa Rais wa Imarati alidai kuwa Mohammed bin Zayed Al Nahyan mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu-Dhabi alifanya juhudi za kufikiwa makubaliano hayo ya amani kati ya Ethiopia na Eritrea na kwamba ubunifu wa bin Zayed ndio uliopelekea kuhitimishwa hitilafu zilizodumu kwa miaka 20 kati ya nchi mbili hizo.
Abiy Ahmed Ali Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye tarehe 8 mwezi huu alifanya safari Eritrea kwa ajili ya makubaliano hayo ya amani alisema katika mazungumzo yake na Rais Isayas Afwerki wa Eritrea, kwamba balozi za nchi hizo mbili zitafunguliwa baada ya kufikiwa makubaliano hayo.
Rais wa Eritrea Isaias Afwerki anatazamiwa kuelekea nchini Ethiopia kesho Jumamosi, siku chache baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Asmara.
Mwaka 1998 hitilafu juu ya umiliki wa maeneo ya mpakani baina ya Ethiopia na Eritrea zilizitumbikiza nchi hizo mbili katika vita vya umwagaji damu vya miaka miwili ambavyo vilisababisha mauaji ya maelfu ya raia wa pande mbili. Mwishoni mwa vita hivyo Ethiopia ilidhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakigombaniwa. Hata hivyo kamati iliyoundwa na Umoja wa Mataifa kushughulikia hitilafu hizo ilihukumu kwamba, neo la Badme ni milki ya Eritrea.