Aliyekuwa mlinzi wa Bin Laden atiwa mbaroni nchini Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46790-aliyekuwa_mlinzi_wa_bin_laden_atiwa_mbaroni_nchini_tunisia
Mlinzi wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Usama bin Laden ametiwa mbaroni nchini Tunisia, baada ya kutimuliwa nchini Ujerumani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2018 02:46 UTC
  • Aliyekuwa mlinzi wa Bin Laden atiwa mbaroni nchini Tunisia

Mlinzi wa aliyekuwa kiongozi wa mtandao wa al Qaida, Usama bin Laden ametiwa mbaroni nchini Tunisia, baada ya kutimuliwa nchini Ujerumani.

Sofiene Sliti, msemaji wa Ofisi ya Mashitaka nchini Tunisia alitoa tangazo hilo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, Sami Idoudi ambaye serikali ya Ujerumani inamtambua kama Sami A anazuiliwa kufuatia agizo la mahakama moja mjini Tunis.

Amesema mshukiwa huyo amekuwa akisakwa na maafisa usalama kwa tuhuma za kuhusika na harakati za ugaidi na misimamo ya kufurutu mipaka alipokuwa nchini Ujerumani.

Idoudi mwenye umri wa miaka 42 na ambaye ameishi nchini Ujerumani kwa zaidi ya miongo miwili, alirejeshwa nchini Tunisia Ijumaa iliyopita, baada ya mchakato mrefu wa kotini kuhusu kutimuliwa kwake.

Abu Sufian bin Qumu, aliyekuwa dereva wa Usama bin Laden

Msemaji wa Ofisi ya Mashitaka nchini Tunisia amesema sheria za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika zinaruhusu raia wa nchi hiyo anayeandamwa na mashitaka ya ugaidi nje ya nchi kurejeshwa nyumbani ili kesi hiyo isikiliziwe nchini humo.

Haya yanajiri mwezi mmoja baada ya askari wa Jeshi la Taifa la Libya kumtia mbaroni Abu Sufian bin Qumu, aliyekuwa dereva wa Usama bin Laden katika jengo moja mjini Derna, baada ya kundi lake la ukufurishaji la Ansar al Sharia kuishiwa na silaha wakati walipokuwa wanapigana na wanajeshi wa Khalifa Haftar.