Waziri Mkuu wa Tunisia akataa kujiuzulu
Waziri Mkuu wa Tunisia amekataa ombi la Rais wa nchi hiyo aliyemtaka ajiuzulu.
Youssef Chahed amesema kuwa kuzungumzia suala la mabadiliko serikalini kutakuwa na taathira mbaya kwa uchumi wa nchi, uwajibikaji wa serikali na katika masuala yanayopewa kipaumbele na serikali hiyo na wakati huo huo kudhoofisha imani ya washirika wa Tunisia.
Waziri Mkuu wa Tunisia ameyasema hayo akijibu maombi yaliyowasilishwa kwake akitakiwa kujiuzulu wadhifa huo. Youssef Chahed amesisitiza kuwa jitihada zinafanywa ili kuondokana na hali ya mgogoro iliyopo kwa kuliwasilisha suala hilo bungeni ili kuweza kupigiwa kura za kuwa na imani naye kwa mara nyingine tena.
Rais Baji Caid Essebsi wa Tunisia majuzi alimtaka Waziri Mkuu huyo ajiuzulu wadhifa huo iwapo mgogoro wa kisiasa na kiuchumi utaendelea nchini humo.
Wakati huo huo Chahed amemtuhumu Hafidh Caid Essebsi mwana wa Rais wa Tunisia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha Nidaa Tunis kuwa amekiuwa chama hicho na akasema mgogoro ndani ya chama hicho umeziathiri pia taasisi za serikali. Itakumbukwa kuwa mwana huyo wa Rais wa Tunisia ameituhumu serikali ya Waziri Mkuu Youssef Chahed kuwa ndiyo iliyosababisha matatizo ya kiuchumi na kutaka kufanyiwa marekebisho serikali hiyo.