Aug 06, 2018 08:05 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Mali alalamikia matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais

Kiongozi wa kambi ya upinzani nchini Mali amelalamikia matokeo ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais na ameamua kupeleka mashtaka mahakamani.

Soumaïla Cissé, mgombea wa urais wa Mali kwa tiketi ya chama cha Union for the Republic and Democracy (URD) amesema kuwa, amefungua mashtaka 20 katika Mahakama ya Katiba kuhusiana na masanduku ya kura, kuvunjwa sheria za uchaguzi na machafuko yaliyozuka katika zoezi zima la uchaguzi huo.

Mgombea huyo ameongeza kuwa, amefungua mashtaka pia dhidi ya majaji sita wa mahakama ambao amesema wanaipendelea serikali.

Upigaji kura nchini Mali

 

Majaji 9 wa Mahakama ya Katiba wana muda wa hadi Jumatano ya wiki hii kuhakikisha wametambua rasmi matokeo ya duru ya kwanza ya urais wa Mali.

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali amepata asilimia 41 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo, huku Soumaïla Cissé wa chama cha upinzani cha URD akiwa amepata asilimia 17 ya kura.

Duru ya kwanza ya uchaugzi wa Mali ilifanyika tarehe 29 Juni mwaka huu na kugubikwa na machafuko na mapigano makubwa ya silaha katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Duru ya pili ya uchaguzi huo inatarajiwa kufanyika tarehe 12 mwezi huu wa Agosti.

Tags