Wanasheria wa Algeria: Ufaransa inapasa kuwalipa fidia wahanga wa ukoloni nchini Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48170-wanasheria_wa_algeria_ufaransa_inapasa_kuwalipa_fidia_wahanga_wa_ukoloni_nchini_algeria
Mwanasheria mmoja wa haki za binadamu nchini Algeria ametaka Paris ilipe gharama na fidia kufuatia kukiri serikali ya Ufaransa kuwatesa na kuwaua wale wote waliokuwa wakiunga mkono mapinduzi ya Algeria.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 16, 2018 02:59 UTC
  • Wanasheria wa Algeria: Ufaransa inapasa kuwalipa fidia wahanga wa ukoloni nchini Algeria

Mwanasheria mmoja wa haki za binadamu nchini Algeria ametaka Paris ilipe gharama na fidia kufuatia kukiri serikali ya Ufaransa kuwatesa na kuwaua wale wote waliokuwa wakiunga mkono mapinduzi ya Algeria.

Muhammad Sami Abdulhamid mwanasheria wa nchini Algeria amesema kuwa Paris inapasa kuzilipa fidia familia za wahanga wa kipindi cha kukoloniwa Algeria na hiyo ni kufuatia Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kukiri na kumuomba radhi mke wa mmoja wa wafuasi wa mapinduzi ya Algeria ambaye aliaga dunia baada ya kuteswa na Wafaransa. 

Maurice Audin alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kifaransa ambaye alikuwa akiishi Algiers mji mkuu wa Algeria miaka kadhaa kabla ya kupata uhuru nchi hiyo; na alikuwa akiunga mkono mapinduzi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa. Wanajeshi wa Ufaransa walimtia mbaroni Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu na aliaga dunia katika mazingira mabaya  baada ya kuteswa vikali na wanajeshi hao. 

Maurice Audin, Mhadhiri wa Algeria katika harakati za ukombozi dhidi ya mkoloni Mfaransa 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Alhamisi iliyopita baada ya kupita miaka 61 ya kupotea Maurice Audin alikwenda nyumbani kwa mke wa mwanamapinduzi huyo na kuiomba radhi familia yake. Ufaransa iliikoloni Algeria kwa miaka 132 na hatimaye nchi hiyo mwaka 1962 ikapata uhuru baada ya miaka kadhaa ya mapambano ya ukombozi ya umwagaji damu. Raia wa Algeria karibu laki tano waliaga dunia katika mapambano ya kuikomboa nchi yao.