Nigeria: Harakati ya Biafra imehusika na mauaji ya watu 55
Polisi ya Nigeria imedai kuwa harakati ya Biafra ndiyo iliyohusika na mauaji ya hivi karibuni ya watu 55, baada ya kugundua kaburi la umati kusini mashariki mwa nchi.
Tony Opuiyo, Msemaji wa Idara ya Ujasusi ya Nigeria amesema uchunguzi wao umebaini kuwa wanachama wa Biafra ndio waliotekeleza mauaji hayo na kufukia miili katika shimo moja kwenye msitu wa Umuanyi katika jimbo la Abia. Amesema kuwa wanachama wa harakati hiyo yumkini waliwaua watu hao baada ya kuwashika mateka kwa siku kadhaa. Msemaji wa Idara ya Polisi ya Siri ya Nigeria amesema kuwa wamewakamata wafuasi kadhaa wa kundi hilo na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi dhidi yao. Mapema mwaka huu, mahakama moja nchini Nigeria ilipinga ombi la kuachiliwa huru kwa dhamana mkuu wa harakati ya Biafra inayopigania kujitenga na Nigeria. Mtandao wa habari wa Africa Time uliripoti habari hiyo na kusema kuwa, mahakama moja nchini humo imekataa ombi la kuachiliwa huru kwa dhamana Nnamdi Kanu, mkuu wa harakati ya kupigania kujitenga na Nigeria eneo la Biafra la kusini mwa nchi hiyo pamoja na watuhumiwa wengine wawili wanaokabiliwa na tuhuma za usaliti. Ifahamike kuwa jimbo la Biafra la kusini mwa Nigeria limeshuhudia vita vibaya sana vya wenyewe kwa wenyewe kwa karibu nusu karne.