Ethiopia yapata rais wa kwanza mwanamke
Bunge la Ethiopia limemuidhinisha mwandiplomasia wa kimataifa, Sahle-Work Zewde kuwa rais wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Sahle-Work ambaye kwa sasa ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu katika Umoja wa Afrika anakuja kurithi mikoba yake Mulatu Teshome Wirtu, ambaye jana Jumatano alilikabidhi bunge la nchi hiyo barua yake ya kujiuzulu.
Ingawaje ofisi ya rais nchini Ethiopia haina nguvu kwani maamuzi mengi muhimu na mamlaka ya nchi hiyo yako mikononi mwa Waziri Mkuu, lakini duru za kitaifa, kieneo na kimataifa zimepongeza uteuzi huo wa Sahle-Work.
Fitsum Arega, Afisa Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmed Abey ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Katika hatua ya kihistoria, mabunge mawili ya nchi hii yamemuidhinisha Shalework Zewde kuwa rais mpya wa Ethiopia. Anakuwa mwanamke wa kwanza kuwa rais katika Ethiopia mpya.

Hatua hii ni katika mlolongo wa mageuzi na mabadiliko yanayofanywa na serikali ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ahmed Abey, tangu aingie madarakani mwezi Aprili mwaka huu.
Wiki iliyopita, Abey alilifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na kuwateua wanawake 10 kuwa mawaziri, na kuifanya nchi hiyo iwe ya tatu baada ya Rwanda na Ushelisheli, kuwa na baraza la mawaziri ambalo asilimia 50 ni wanawake barani Afrika.