Basi lililokuwa likielekea A/Kusini laripuka na kuua abiria 43 Zimbabwe
(last modified Fri, 16 Nov 2018 14:40:47 GMT )
Nov 16, 2018 14:40 UTC
  • Basi lililokuwa likielekea A/Kusini laripuka na kuua abiria 43 Zimbabwe

Watu wasiopungua 43 wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya basi la abiria kuripuka na kushika moto usiku wa kuamkia leo nchini Zimbabwe.

Charity Charamba, msemaji wa Polisi ya Zimbabwe amesema leo Ijumaa kuwa, basi hilo lilikuwa likielekea katika nchi jirani ya Afrika Kusini na kwamba makumi ya abiria wengine wamejeruhiwa kwenye ajali hiyo.

Duru za habari zinaarifu kuwa, yumkini mtungi wa gesi wa mmoja wa abiria uliripuka ndiposa basi hilo likashika moto na kuungua hadi likabakia majivu.

Mashuhuda wanasema ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu ya Beitbridge kuelekea Bulawayo.

Ajali za barabarani hutokea mara kwa mara nchini Zimbabwe, kutokana na ubovu wa barabara tena zilizojaa mashimo, na kutoheshimiwa sheria za barabarani.

Haya yanajiri wiki moja baada ya watu wengine 47 kufariki dunia katika ajali nyingine iliyohusisha mabasi mawili ya abiria. Mabasi hayo yaligongana ana kwa ana katika barabara iliyoko katikati ya mji mkuu Harare na mji wa Rusape.

Aidha Juni mwaka jana, watu wengine 43 waliaga dunia katika ajali nyingine iliyohusisha basi la abiria kaskazini mwa nchi, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Zambia.