Jeshi la Sudan latangaza uungaji mkono kwa al Bashir, vyama vya upinzani vyajiunga na maandamano ya wananchi
(last modified Tue, 25 Dec 2018 02:59:40 GMT )
Dec 25, 2018 02:59 UTC
  • Jeshi la Sudan latangaza uungaji mkono kwa al Bashir, vyama vya upinzani vyajiunga na maandamano ya wananchi

jeshi la Sudan limetangaza uungaji mkono wake kwa kiongozi anayezongwa na matatizo mengi ya kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo baada ya kushadidi maandamano ya wananchi wanaopinga hali mbaya ya uchumi. Waandamanaji hao pia wametoa wito wa kuondolewa madarakani serikali ya sasa ya Khartoum.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Sudan imesema kuwa, taasisi hiyo inamuunga mkono Rais Omar Hassan al Bashir na matunda ya taifa la nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi la Sudan imesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi zote za usalama likiwemo Jeshi la Polisi, Kikosi cha Radiamali ya Haraka na Idara ya Upelelezi ya Taifa kwa ajili ya kukabiliana na waandamanaji.

Awali Mkuu wa Idara ya Upelelezi ya Sudan alidai kuwa waasi wenye uhusiano na utawala haramu wa Israel ndio wanaochochea maandamano yanayoendelea kwa siku kadhaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Wasudan wanapinga sera za kiuchumi za Rais al Bashir

Salah Abdallah Gosh amesema mtandao wenye makao yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambao una uhusiano na Israel umeingiza mamia ya waasi nchini Sudan kwa shabaha ya kuchochea machafuko nchini humo.

Mkuu wa vyombo vya upelelezi vya Sudan amesema kuwa vyombo vya usalama vimewatia nguvuni watu kadhaa ambao ni sehemu ya wafuasi 280 wa kundi la waasi la Abdul Wahid Mohamed Nur walioingizwa Sudan kupitia Nairobi.

Zaidi ya waandamanaji 22 wameuawa hadi sasa katika Maandamano ya Mkate nchini Sudan ambapo wananchi wanapinga hali mbaya ya uchumi na ughali wa bidhaa. 

Tags