Jan 02, 2019 15:16 UTC
  • Msalaba Mwekundu: Mamia ya Wakongomani wamekimbilia Uganda

Shirika la Msalaba Mwekundu limesema mamia ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekimbilia nchini Uganda baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa Jumapili iliyopita.

Msemaji wa shirika hilo nchini Uganda, Irene Nakasiita amesema leo Jumatano kwamba kuna wasiwasi mkubwa wa kueneo ugonjwa wa Ebola katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutokana na wimbi hilo la wakimbizi wanaotoka Kongo DR.

Amesema baadhi ya Wakongomani wamerejeshwa nchini kwao baada ya kukataa kukaguliwa na maofisa wa Wizara ya Afya ya Uganda katika mpaka wa nchi mbili hizo.

Itakumbukwa kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI iliakhirisha uchaguzi wa rais na wa bunge mjini Beni, mashariki mwa nchi kutokana na homa ya Ebola. 

Chanjo ya Ebola nchini Kongo DR

Alkhamisi iliyopita, watu 24 wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola walitoroka kituo cha matibabu mjini Beni baada ya kituo hicho kushambuliwa na watu waliokuwa wakipinga kuakhirishwa uchaguzi huo katika mji huo.

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka uliomalizika wa 2018, kulikuwa kumeripotiwa kesi zaidi ya 600 za Ebola, huku watu 350 wakiripotiwa kufariki dunia kutokana na homa hiyo hatari kaskazini mashariki mwa DRC.

Tags