Feb 22, 2019 17:12 UTC
  • Watetezi wa haki za binadamu waandamana kupinga hukumu za vifo Misri

Watetezi wa haki za binadamu wamefanya maandamano katika nchi kadhaa duniani kupinga utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya wapinzani wa serikali ya Misri.

Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu katika miji ya Tunis na Berlin walikusanyika katika miji hiyo wakilaani hukumu ya kifo iliyotekelezwa nchini Misri dhidi ya wapinzani wa mapinduzi ya serikali halali ya nchi hiyo katika kadhia inayojulikana katika vyombo vya habari kuwa ni ya mauaji ya aliyekuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo, Hisham Barakat.

Waandamanaji hao wanasema hukumu za vifo dhidi ya wapinzani hao hazikutegemea misingi sahihi na ya kiadili ya mahakama.

Watetezi wa haki za binadamu wanalaani utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya wapiznani Misri.

Waandamanaji hao ambao walikusanyika mbele ya ubalozi wa Misri mjini Tunis, Tunisia wametoa nara dhidi ya utawala wa kijeshi wa Misri na kutoa wito wa kusitishwa mauaji ya wapinzani na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu.

Waandamanaji hao pia wamezitaka taasisi na jumuiya za kimataifa kukabiliana ipasavyo na ukatili unaofanyika nchini Misri dhidi ya wapinzani wa serikali ya Jenerali Abdel Fattah al Sisi.

Maandamano kama hayo yamefanyika pia Berlin nchini Ujerumani ambako washiriki wameitaka jamii ya kimataifa kukomesha kimya chake na kukemea ukiukaji wa haki za binadamu nchini Misri. Waandanaji hao wametoa wito wa kuondolewa madarakani serikali ya al Sisi, na kusitishwa hukumu ya kifo dhidi ya wapinzani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza pia imepinga utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi ya wapinzani wa utawala wa Abdel Fattah al Sisi nchini Misri na kusema London inapinga hukumu hiyo.

Siku chache zilizopita maafisa wa serikali ya Misri waliwanyonga watu tisa kwa madai ya kupatikana na hatia ya mauaji ya aliyekuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo, Hisham Barakat aliaga dunia mwaka 2015.

Watu hao tisa walionyongwa ni miongoni mwa watuhumiwa 28 ambao walihukumiwa kifo katika kesi hiyo mwaka 2017.

Tags