Tanzania yatakiwa kuangalia upya sheria zinazokandamiza wanawake
(last modified Fri, 08 Mar 2019 07:58:28 GMT )
Mar 08, 2019 07:58 UTC
  • Tanzania yatakiwa kuangalia upya sheria zinazokandamiza wanawake

Huku Tanzania ikijiunga na nchi nyingine duniani katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake inayoadhimishwa hii leo, serikali ya Dar es Salaam imetakiwa kuangalia upya sera na sheria zinazohusu wanawake ili kuimarisha ustawi wao.

Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga ambapo amebainisha kuwa, serikali ya Tanzania inapaswa kufanyia marekebisho baadhi ya vifungu vilivyo na mapungufu na vinavyokandamiza haki za wanawake katika sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mirathi.

Ameongeza kuwa, “Ni vizuri tukawa na sera na sheria nzuri kwa wanawake. Sheria hizo zitasaidia wanawake kuwa na ustawi. Sheria za mirathi na zinazohusu ukatili wa wanawake zifanyiwe marekebisho.” 

Aidha Henga ameitaka jamii kubadilisha mtazamo na fikra hasi dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na kupiga vita mfumo-dume, na badala yake iheshimu na kutimiza haki za wanawake.

Siku ya Wanawake Duniani

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu anasisitiza kuwa mtazamo chanya juu ya wanawake utaleta amani, maendeleo na mafanikio kwa jamii.

Mwaka 1977 Umoja wa Mataifa uliitangaza rasmi Machi 8 kuwa Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa. Awali siku hii ilianzishwa kama tukio la kisiasa la kisoshalisti lakini baadaye liliingia katika utamaduni wa nchi nyingi duniani.

Tags