Rais al Bashir wa Sudan atoa amri ya kuwastaafisha maafisa wa jeshi
(last modified Sat, 09 Mar 2019 07:31:12 GMT )
Mar 09, 2019 07:31 UTC
  • Rais al Bashir wa Sudan atoa amri ya kuwastaafisha maafisa wa jeshi

Rais Omar al Bashir wa Sudan ametoa amri ya kuwastaafisha maafisa kadhaa wa jeshi la nchi hiyo.

Hatua hiyo ya al Bashir ilichukuliwa jana Ijumaa ambapo maafisa wengi wa jeshi la nchi hiyo wamestaafishwa na baadhi yao wamepandishwa vyeo.

Taarifa ya jeshi la Sudan imesema kuwa, maafisa hao wa kijeshi waliopandishwa vyeo ni wa daraja tofauti.

Wakati huo huo jeshi hilo la Sudan limedai kuwa hiyo ni hatua ya kawaida iliyokuwa imepangwa tangu zamani.

Maandamano ya kumpinga Rais Omar al Bashid nchini Sudan

 

Amri hiyo ya kustaafishwa maafisa wa kijeshi imetolewa na al Bashir katika hali ambayo karibu miezi mitatu sasa Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi ambao wanamtaka al Bashir ang'oke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miaka 30 sasa.

Taarifa zinasema kuwa makumi ya watu wameuawa wakiwemo maafisa wa polisi na mamia ya wengine wamejeruhiwa katika machafuko yaliyotokea kwenya maandamano hayo ya wananchi wa Sudan.

Wakati huo huo televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza kuwa, kukosekana uongozi maalumu wa wimbi hilo kubwa la maandamano ya wananchi huko Sudan kunakwamisha mazungumzo baina ya wananchi hao na serikali. 

Tags