Waziri wa Afya Tunisia ajiuzulu baada ya watoto 11 kufa hospitalini
Waziri wa Afya wa Tunisia Abdel-Raouf El-Sherif amejiuzulu Jumamosi baad aya watoto 11 kufariki hospitalini bila sababu maalumu katika hospitali moja mjini Tunis.
Duru zinaarifu kuwa watoto hao wamefariki kwa sababu zisizojulikana katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita. Wakuu wa wizara ya afya na waendesha mashtaka wameanzisha uchunguzi kuhusu vifo hivyo huku baadhi wakisema chanzo chake ni matitzo ya damu yaliyotokana na uzembe.
Watunisia wamekuwa wakilalamika kuwa huduma za afya nchini humo zinaendelea kudhoofika na kwamba sekta ya afya inakumbwa na ufisadi mkubwa na pia wafanyakazi wa sekta hiyo hawapati mishahara ya kutosha.
Mwaka jana pia wanafunzi wanaosomea taaluma ya udakitari nchini Tunisia walifanya maandamano nje ya ofisi ya Wizara ya Afya wakishinikiza kutekelezewa matakwa yao.
Mgogoro wa kiuchumi umevuruga viwango vya maisha nchini Tunisia. Kiwango cha watu wasio na kazi ni kikubwa kama ambavyo mkwamo wa kisiasa nao umezuia marekebisho ya kuvutia wawekezaji na kuandaa nafasi mpya za kazi. Serikali ya Tunisia imechukua hatua za marekebisho ya kiuchumi ili kuwafurahisha wafadhili na wakopeshaji kama vile IMF, tab'an inaonekana marekebisho hayo ni kwa madhara ya mwananchi wa kawaida.