Algeria; kuendelea mgogoro au kufanya harakati katika njia ya demokrasia?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52124-algeria_kuendelea_mgogoro_au_kufanya_harakati_katika_njia_ya_demokrasia
Baada ya wiki kadhaa za malalamiko, maandamanao na kushadidi hali hiyo katika siku za hivi karibuni baada ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria kutangaza kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tano mtawalia, hatimaye kiongozi huyo amefutilia mbali uamuzi wake huo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 13, 2019 02:25 UTC
  • Algeria; kuendelea mgogoro au kufanya harakati katika njia ya demokrasia?

Baada ya wiki kadhaa za malalamiko, maandamanao na kushadidi hali hiyo katika siku za hivi karibuni baada ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria kutangaza kugombea kiti cha urais kwa muhula wa tano mtawalia, hatimaye kiongozi huyo amefutilia mbali uamuzi wake huo.

Mbali na kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, Abdelaziz Bouteflika ametangaza kuakhirishwa uchaguzi huo. Uchaguzi wa rais nchini Algeria ulipangwa kufanyika tarehe 18 ya mwezi ujao wa Aprili, lakini sasa kufuatia tangazo la Bouteflika uchaguzi huo umeakhirishwa. Katika ujumbe wake, Rais wa Algeria ametangaza kuwa, anadiriki vyema ujumbe wa harakati ya malalamiko ya wananchi na ameahidi kufanya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitaasisi katika fremu ya kutazama upya Katiba na kufanyika kura ya maoni. Hata hivyo, Rais Bouteflika hajatangaza tarehe mpya ya kufanyika uchaguzi na kutekeleza ahadi alizotoa.

Tangu mwezi Februari uliopita, Algeria imegeuka na kuwa uwanja wa maandamano ya wananchi na vyama vya siasa vinavyompinga Rais Bouteflika. Akthari ya wapinzani walikuwa wakipinga Bouteflika kugombea tena muhula wa tano kutokana na umri mkubwa, uzee na kutokuwa na afya ya kimwili.

Maandamano ya wananchi wa Algeria

Kadhalika wapinzani wengi nchini Algeria wanakosoa vikali utendaji wa kisiasa na kiuchumi wa serikali yake hususan katika miaka ya hivi karibuni. Kutekelezwa mipango ya ustawi na maendeleo nchini Algeria, kuzingatiwa vijana na wanawake na kuboreshwa hali ya uchumi wa nchi ni miongoni mwa matakwa muhimu ya wananchi wa nchi hiyo. Katika uga wa kisiasa pia, wapinzani wanataka kuongezwa uhuru wa kisiasa na kiraia na kuweko wigo mpana wa harakati za kidemokrasia.

Licha ya kuwa, vyama vingi vya siasa na wapinzani wamefurahishwa mno na tangazo la Rais Bouteflika la kujitoa katika kinyang'anyiro cha kuwania kiti cha urais katika uchaguzi ujao, lakini hatua yake ya kuakhirisha uchaguzi na kutoa ahadi hizi na zile, imeleta hofu na matumaini kwa mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo. Akthari ya wanasiasa na wananchi wa Algeria wameingiwa na wasiwasi kutokana na kuakhirishwa uchaguzi na wanasema kuwa, hatua hiyo inakinzana na misingi ya demokrasia na kwamba, kuakhirishwa uchaguzi kunafungua njia ya kuendelea kubakia zaidi madarakani Bouteflika na chama chake.

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ambaye amekuwa akitembelea kiti cha magurudumu

Ahmad Adhimi, msemaji wa chama cha Talae El-Hurriyat amebainisha kuwa, lengo la maamuzi haya ya Bouteflikak ni kununua muda na kudhamini kuendelea kubakia madarakani serikali yake na kuongeza kuwa, uamuzi wa Rais wa Algeria wa kufuta na kuakhirisha uchaguzi, si halali na maamuzi haya ni zile zile ahadi ambazo alizitoa mwaka 2011 na hakuzitekeleza.

Baadhi ya wanasiasa wanasema kuwa, uamuzi wa Rais Bouteflika umechukuuliwa katika fremu ya demokrasia na ni matokeo ya malalamiko ya mwezi mmoja katika nchi hiyo na wanaamini kwamba, hatimaye kilio cha waandamanaji kimesikilizwa. Kundi la wanasiasa hawa linaamini kwamba, takwa la waandamanaji lillikuwa ni kutogombea tena kiti cha Urais Abdelaziz Bouteflika  mwenye umri wa miaka 82 na ambaye ni mgonjwa, takwa ambalo limetekelezwa.

Maandamano ya wananchi wa Algeria ambayo yamemlazimisha  Rais Bouteflika afute uamuzi wake wa kugombea urais

Abdul-Ali Razaqi, mhadhiri wa Chuo Kikuu nchini Algeria anasema: Haifahamiki kwa sasa ni nani hasa anayeongoza nchini humo. Mimi ninaweza kusema kinagaubaga kwamba, katu vijana wa Algeria hawamtaki kiongozi yeyote yule miongoni mwa wanaotawala hivi sasa nchini humo, kwani sisi tumeingia katika hatua ambayo inajulikana kama 'uasi wa raia'.

Filihali inawezekana kusema kuwa, kujitoa Abdelaziz Bouteflika katika kinyang'anyiro cha kuwania Urais nchini Algeria inahesabiwa kuwa hatua nzuri katika matukio ya kisiasa ya nchi hiyo. Lakhdar Brahimi, mwanasiasa mkongwe wa Algeria sanjari na kuonyesha kuridhishwa na hatua ya Bouteflika ya kujiondoa kugombea Urais amesema kuwa, kwa hatua hiyo sasa Algeria imeingia katika hatua mpya. Katika mazingira kama haya, hofu na matumaini vingali vimeugubika mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.