Msaada wa dola milioni 20 kufuatia maafa ya mafuriko kusini mwa Afrika
(last modified Thu, 21 Mar 2019 07:40:42 GMT )
Mar 21, 2019 07:40 UTC
  • Msaada wa dola milioni 20 kufuatia maafa ya mafuriko kusini mwa Afrika

Watu zaidi ya 500 wamthibitishwa kupoteza maisha Zimbabwe, Malawi na Msumbiji kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na kimbuga Idai na kuwaacha maelfu bila makazi na hivyo wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu. Kufuatia hali hiyo, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa umetangaza kutoa msaada wa dola milioni 20 kusaidia waathirika.

Kwa mujibu wa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Mark Lowcock mfuko huo wa dharura CERF umetangaza kutenga dola miloni 20 kwa ajili ya kupiga jeki msaada wa kibinadamu kufuatia Kimbunga Idai kilichokumba nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi huku kipaumblele ikitolewa kwa Msumbiji iliyoathirika zaidi na ambayo imetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kuanzia jana Machi 20 ili kuzika waliopoteza maisha.

Kupitia taarifa ya OCHA, Lowcock amesema fedha hizo zitatumika kuimarisha juhudi za mamlaka ya nchi hizo tatu ikiwemo kwa kutoa huduma ya afya, usalama wa chakula, ulinzi, lishe bora na elimu .

Aidha mkuu huyo wa OCHA amesema makundi ya watu walio hatarini ikiwemo watoto, wanawake wajawazito na wanaonyonyesha, watu wanoishi na ulemavu na walio na magonjwa ya muda mrefu ndio watakaopewa kipaumbele.

Maziko ya walioaga dunia kutokana na mafuriko Msumbiji

OCHA imesema fedha hizo pia zitasaidia mashirika ya kibinadmu kuimarisha mipango yao ikiwemo mbinu za kuwasiliana na kuimarisha huduma za maji na huduma za dharura za afya kwa ajili ya kupunguza hatari ya magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji na viini.

Lowcock hatahivyo amesema mgao huo kutoka kwa CERF ni wa kukabiliana na dharura za hivi sasa lakini hautoshi kuweza kukabiliana na mahitaji ambayo yanatarajiwa kuimarika na hiyvo ametoa wito kwa wafadhili kuchangia fedha kwa ajili ya watu walioathirka kufuatia kupigazkwa kimbunga Idai.

Kimbunga Idai kilipiga mji wa Beira katika jimbo la Sofala katikati mwa Msumbiji usiku wa Machi 14 na 15 ambapo kabla ya hapo kulishuhudiwa mvua kubwa na mafuriko katika nchi tatu ikiwemo Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha maelfu ya watu kufurushwa makwao na vifo na uharibifu wa mali.