Guterres ataka kuharakishwa utekelezwaji wa makubaliano ya amani CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52369-guterres_ataka_kuharakishwa_utekelezwaji_wa_makubaliano_ya_amani_car
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa pande zote husika kutekeleza kwa haraka mapatano ya amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliyotiwa saini katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, siku moja baada ya kuundwa serikali mpya inayoyajumuisha makundi ya wabeba silaha.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Mar 24, 2019 03:29 UTC
  • Guterres ataka kuharakishwa utekelezwaji wa makubaliano ya amani CAR

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa pande zote husika kutekeleza kwa haraka mapatano ya amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yaliyotiwa saini katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui, siku moja baada ya kuundwa serikali mpya inayoyajumuisha makundi ya wabeba silaha.

Katika taarifa, Antonio Guterres amesema, "Naziomba pande zote za makubaliano hayo ya amani kuheshimu vipengee vyote walivyoviidhinisha, hususan kujiepusha na ghasia na kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utu."

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Firmin Ngrébada, siku ya Ijumaa alitangaza baraza jipya la mawaziri muda mfupi baada ya kuwasili Bangui akitokea mjini Addis Ababa, Ethiopia alikoshiriki mkutano wa mazungumzo ya amani ya nchi yake.

Katika baraza lake jipya, Ngrébada amehakikisha wapinzani na makundi yote ya wabeba silaha yanapata nafasi za uongozi, hata kama nafasi muhimu zimechukuliwa na upande wa serikali pekee.

Mwezi uliopita, rasimu ya awali ya mapatano hayo ya amani yalitiwa saini na wajumbe wa serikali pamoja na wawakilishi wa makundi 14 ya waasi katika kikao kilichohudhuriwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Parfait Onanga Anyanga, Rais wa CAR Faustin Archange Touadera na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, AU, Moussa Faki Mahamat, baada ya makubaliano yaliyofikiwa mjini Khartoum nchini Sudan wiki moja kabla.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Firmin Ngrébada

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka nchini humo.

Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na lile la Seleka. Hali hiyo imezidi kuisababishia matatizo mengi Jamhuri ya Afrika ya Kati.