WHO yatahadharisha kuhusu kuibuka maradhi ya kipindupindu nchini Msumbiji
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuhusiana na kuibuka wimbi la pili la maradhi ya kipindupindu na maradhi mengine katika nchi ya Msumbiji iliyopigwa na kimbunga cha Idai hivi karibuni.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeashiria kimbunga cha Idai kilichoikumba Msumbiji hivi karibuni pamoja na nchi za Zimbabwe na Malawi na kueleza kwamba, kuna wasiwasi wa kuibuka maradhi ya kipindupindu nchini Msumbiji.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kuwa, kuna ulazima wa kupelekwa misaada ya haraka ya kibinadamu kwa watu milioni moja na laki nane walioathiriwa na mafuriko yaliyotokana na kimbunga cha Idai nchini Msumbiji.
WHO imeeleza kuwa, inahitajia bajeti ya dharura ya kiasi cha dola milioni 182 kwa ajili ya kuwasaidia waathiriwa wa janga hilo la kimaumbile katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Zaidi ya watu 700 wamethibitishwa kupoteza maisha hadi hivi sasa kutokana na kimbunga kikali cha Idai kilichopiga eneo la kusini mwa Afrika huku taarifa zikisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka idadi hiyo kutokana na watu wengi kutojulikana waliko.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, uharibifu wa janga hilo la kimaumbile ni mkubwa sana kiasi kwamba, umefika umbali wa kilomita 300 kutoka eneo kilipopiga kimbunga cha Idai.
Mamia ya nyumba zimeharibiwa kikamilifu katika mji wa Beira uliopigwa moja kwa moja na kimbunga hicho huko nchini Msumbiji huku miundombinu kama barabara zikiharibiwa.