Kenya na Somalia zasuluhisha mzozo wa kidiplomasia, zawarejesha mabalozi
Kenya na Somalia zimesuluhisha mzozo wa kidiplomasia baina yao, uliochochewa na mgogoro kuhusu mpaka wa pamoja wa bahari.
Jana Jumatano mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili hizo walifanya mazungumzo jijini Nairobi, na pande mbili hizo zikakubalina kuwarejesha mabalozi wao katika miji mikuu ya nchi hizo, walioitwa nyumbani kufuatia mgogoro huo mwezi Februari mwaka huu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imetoa taarifa inayosema kuwa, "Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Monica Juma na mwenzake wa Somalia, Ahmed Issa Awad wamekutana na kufanya mazungumzo ya kina kuhusu mgogoro wa mpaka wa baharini katika Bahari ya Hindi, wenye urefu wa maili mraba 62,000. Pande mbili zimesisitizia haja ya kuurejesha katika hali ya kawaida uhusiano wao wa kidiplomasia kwa kuwarejesha mabalozi katika nafasi zao, kama hatua ya kwanza ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo."
Katikati ya mwezi Februari mwaka huu, Kenya ilimfukuza balozi wa Somalia mjini Nairobi huku ikimuita nyumbani balozi wake wa Mogadishu, ikiituhumu nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kuwa imepiga mnada maeneo yake yenye gesi na mafuta katika mpaka wao wa pamoja wa baharini.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya ilisema, "Unyakuzi wa rasilimali za Kenya kinyume cha sheria hauwezi kupita hivi hivi bila kupewa jibu, na kitendo hicho kinahesabiwa kama uvamizi dhidi ya wananchi wa Kenya na rasilimali zao."
Somalia ilikanusha madai kuwa imepiga mnada maeneo hayo ya Kenya, na kusisitiza kuwa faili la mgogoro wa mpaka wao wa pamoja wa baharini linashughulikiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).