Watoto Karibu Laki Nne Msumbiji wanahitaji msaada, mvua kuendelea
(last modified Sun, 28 Apr 2019 14:32:56 GMT )
Apr 28, 2019 14:32 UTC
  • Watoto Karibu Laki Nne Msumbiji wanahitaji msaada, mvua kuendelea

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limeonya kwamba watoto na familia zao nchini Msumbiji wanaweza kukabiliwa na hatari ya kifo kutokana na mafuriko makubwa na maporomoko.

Hatari hiyo imebainika baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa WMO kuonya kwamba mvua kubwa itaendelea kunyesha.

Kwa mujibu wa UNICEF watoto 368,000 hivi sasa wako hatarini nchini Msumbiji na wanaweza kuhitaji msaada wa kibinadamu. Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika juma hili imekumbwa na kimbunga cha pili Kenneth ikiwa ni wiki sita tu baada ya kimbunga Idai kusambaratisha mji wa Beira na viunga vyake na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwemo kupotea kwa maisha ya watu na miundombinu.

Mamlaka nchini Msumbiji imethibitisha kwamba hadi kufikia sasa watu watano wamepoteza maisha kutokana na kimbunga Kenneth.

Kimbunga Kenneth kiliwasili Alhamisi wiki hii Cabo Delgado katika jimbo la Kaskazini mwa Msumbiji kikiwa na kasi ya daraja la 4 na watabiri wameonya kwamba mvua kubwa itaendelea kunyesha kwa siku kadhaa zijazo na kuyaweka katika hatari kubwa ya mafuriko na maporomoko ya udongo maeneo yaliyoathirika.

Hasara iliyosababishwa na mafuriko Msumbiji

UNICEF pia imesisitiza kwamba hofu kubwa kwa sasa ni watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine hasa ukizingatia kwamba kimbunga hicho kimeharibu asilimia 90 ya nyumba katika baadhi ya vijiji. Cabo Delgado haina historia ya vimbunga hivyo hofu ni ya haraka kwamba jamii katika eneo hilo hawajajiandaa na kiwango hicho cha kimbunga na hivyo kuwaweka Watoto na familia katika hatari kubwa.