May 03, 2019 13:41 UTC
  • CAFOMI: Wahamiaji haramu kutoka DRC yumkini wakaeneza Ebola Uganda

Uganda imejiweka katika hali ya tahadhari kutokana na kuongezeka wasiwasi juu ya uwezekano wa kuenea hadi nchini humo ugonjwa hatari wa Ebola kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo inapambana na mlipuko wa homa hiyo.

Shirika la masuala ya kibinadamu la kuwasaidia wahajiri CAFOMI lenye makao yake jijini Kampala limesema malaki ya Wakongomani wanaokimbia vita na mapigano mashariki mwa Kongo DR na kuingia nchini Uganda wanaliweka taifa hilo la Afrika Mashariki katika hatari ya kukumbwa na wimbi la maambukizi ya Ebola.

Mkurugenzi Mkuu wa CAFOMI, Francis lwa amesema leo Ijumaa kuwa, katika hali ambayo baadhi ya wahajiri wa DRC wanapewa hifadhi baada ya kufuata taratibu zote za kisheria, kuna baadhi wanaingia nchini Uganda kinyume cha sheria, na kutumiwa kama ngao ya kibinadamu na magege yanayobeba silaha wanaowazuia kujisajili mpakani.  

Zaidi ya watu 60,000 wameyakimbia makazi yao katika mji wa Beni mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Kongo DR, tangu wimbi jipya la mashambulizi ya magenge yanayobeba silaha lianze Machi 30.

Naye Musa Ecweru, Waziri wa Kupambana na Majanga na Masuala ya Wakimbizi wa Uganda amesema, "Uganda itaendelea kufungua milango yake kwa ajili ya wakimbizi kwa kuwa hiyo ni katika sera zake. Hata hivyo wahamiaji wa DRC wanaovuka mpaka wa nchi hizo na kuingia Uganda kinyume cha sheria wanaiweka nchi hii katika hatari ya kukabiliwa na ueneaji wa virusi vya Ebola. Wahajiri hao wanapaswa kusajiiwa na Idara ya Uhamiaji sambamba na kukaguliwa na Wizara ya Afya kabla kuruhusiwa nchini."

Ramani ya Uganda

Juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeendelea kukabiliwa na vizingiti kutokana na makundi ya waasi kushambulia vituo vya afya vinavyotoa matibabu kwa wagonjwa wa maradhi hayo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, watu 957 wameaga dunia kutokana na maradhi ya Ebola nchini humo tangu ugonjwa huo hatari uibuke upye Agosti mwaka jana.

Tags