Tripoli yatishia kuyafutia leseni mashirika ya kigeni nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53403-tripoli_yatishia_kuyafutia_leseni_mashirika_ya_kigeni_nchini_libya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya (GNA) yenye makao yake Tripoli na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa imetishia kuyapokonya leseni mashirika 40 ajinabi likiwemo shirika la mafuta la Ufaransa Total yanayohudumu nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2019 21:48 UTC
  • Tripoli yatishia kuyafutia leseni mashirika ya kigeni nchini Libya

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya (GNA) yenye makao yake Tripoli na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa imetishia kuyapokonya leseni mashirika 40 ajinabi likiwemo shirika la mafuta la Ufaransa Total yanayohudumu nchini humo.

Wizara ya Uchumi na Viwanda ya serikali hiyo ya Tripoli inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj imeyataka mashirika hayo ya kigeni nchini humo kusajili upya leseni zao ndani ya muda wa miezi mitatu ijayo, vinginevyo yatafutiwa vibali  vya kuendelea kuhudumu nchini humo.

Wadadisi wa mambo wanasema hatua hiyo ya serikali ya Tripoli inakusudia kuyashinikiza mashirika hayo ajinabi hususan ya Ufaransa yaache kuviunga mkono vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya, Fathi Bashagha alisema Ufaransa inamuunga mkono jenerali huyo muasi Khalifa Haftar mwenye makao yake katika mji wa Benghazi, na ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kijeshi ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli.

Operesheni ya vikosi vya Haftar ya kuuteka mji wa Tripoli

Tarehe 4 Aprili mwaka huu, Jenerali Haftar alitoa amri kwa wapiganaji wake ya kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa Libya kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na Ufaransa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu 430 wameshauawa na zaidi ya 2000 wengine wamejeruhiwa tangu yalipoanza mashambulizi hayo, mbali na watu 55 elfu wengine kukimbia makazi yao kutokana na vita hivyo.