Kenya na Somalia zaendelea kuvutana, Mogadishu yafuta mikutano ya Nairobi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53745-kenya_na_somalia_zaendelea_kuvutana_mogadishu_yafuta_mikutano_ya_nairobi
Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kushtadi mvutano kati ya Kenya na Somalia, serikali ya Mogadishu imejibu mapigo na kufuta mikutano yake iliyotazamiwa kufanyika jijini Nairobi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2019 02:51 UTC
  • Kenya na Somalia zaendelea kuvutana, Mogadishu yafuta mikutano ya Nairobi

Katika kile kinachoonekana ni kuendelea kushtadi mvutano kati ya Kenya na Somalia, serikali ya Mogadishu imejibu mapigo na kufuta mikutano yake iliyotazamiwa kufanyika jijini Nairobi.

Hii ni baada ya maafisa watatu wa serikali ya Somalia wakiwa na hati za kusafiria za kidiplomasia kuzuiwa kuingia nchini Kenya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Idara ya Uhamiaji ilidai kuwa, Waziri Msaidizi wa Maji na Nishati wa Somalia, Osman Liban pamoja wabunge Ilyas Ali Hassan na Zamzam Dahir walizuiwa kuingia nchini humo kwa kuwa hawakuwa na viza.

Katika kujibu mapigo, serikali ya Mogadishu sambamba na kufuta mikutano yake ijayo iliyotazamiwa kufanyika Nairobi, imeziagizi asasi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazohudumu katika maeneo mbali mbali ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika zihamishie ofisi zao jijini Mogadishu, vinginevyo zintapokonywa leseni za kuhudumu.

Akthari ya asasi hizo zina mfungamano wa moja kwa moja na mashirika ya Kenya.

Jana Jumapili, Wizara ya Afya ya Somalia iliziandikia barua taasisi za Umoja wa Mataifa na wafadhili wao ikiwataka wapange upya mikutano iliyokuwa imepangwa kufanyika Nairobi.

Mpaka wa baharini unaozozaniwa na Kenya na Somalia

Mkurugenzi Mkuu wa wizara hiyo, Abdullahi Hashi Ali amesema katika barua hiyo kuwa, "Kutokana na matatizo ya hivi karibuni ya kusafiri jijini Nairobi Kenya, hatutaweza kushiriki mikutano, warsha na vikao vijavyo vilivyokuwa vimepangwa kufanyika katika mji huo. Tunashauri mikutano hiyo ifanyike nchini hapa au nchi mbadala ili kuwepesisha suala la usafiri."

Vuta nikuvute kati ya Kenya na Somalia iliibuka baada ya kuripuka taarifa kuwa Somalia imepiga mnanda maeneo yenye utajiri wa mafuta na gesi katika eneo linalozozoaniwa baina ya nchi mbili eneo la mpaka katika Bahari ya Hindi.