Jun 01, 2019 11:22 UTC
  • Watu 16 wauawa katika shambulizi la kigaidi nchini Msumbiji

Kwa akali watu 16 wameuawa katika shambulizi jipya la kigaidi lililotokea huko kaskazini mwa Msumbiji.

Mwalimu mmoja ambaye alishuhudia hujuma hiyo na ambaye hakutaka kutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, magaidi waliokuwa wamejizatiti kwa silaha walifanya ukatili huo Jumanne iliyopita katika mji wa pwani wa Macomia, katika eneo la Cabo Delgado kaskazini mwa nchi.

Duru za habari zinaarifu kuwa, miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo ni wanajeshi watatu wa serikali.

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Maafisa usalama wa Msumbiji wakifanya msako

Genge hilo la kitakfiri limekuwa likifanya mashambulizi hayo licha ya serikali ya Msumbiji kutuma wanajeshi na polisi katika maeneo hayo ambayo yapo katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania.

Tayari mamia ya washukiwa wa ugaidi wakiwemo raia wa Tanzania wamekamatwa na kupandishwa kizimbani.

 

Tags