Wafadhili waahidi dola bilioni 1.2 kuisaidia Msumbuji baada ya vimbunga
Jumla ya dola bilioni 1.2 zimechangishwa mjini Beira katika mkutano wa kimataifa wa siku mbili wa ufadhili kwa ajili ya ujenzi mpya wa kijamii, uzalishaji na miundombinu nchini Msumbiji baada ya taifa hilo kuathirika vibaya na vimbunga mapema mwaka huu.
Msumbiji inahitaji dola bilioni 3.2 kwa ajili ya kuyasaidia majimbo yaliyosambaratishwa vibaya na vimbunga Idai na Kenneth. Majimbo yaliyoathirika zaidi ni pamoja ya Sofala, Manica, Tete, Zambezia, Inhambane, Nampula na Cabo Delgado.
Akizungumza baada ya mchango huo, Rais Filipe Nyusi wa Msumbuji aliwashukuru sana wafadhili wote kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya watu wa msumbuji.
Katika mkutano huo wa kimataifa ulioandaliwa na serikali ya Msumbiji na kuwezeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, Muungano wa Ulaya na Benki ya Dunia ni miongoni mwa waliochangia kiasi kikubwa cha fedha. Muungano wa Ulaya umetoa dola milioni 200, kati ya hizo dola milioni 100 zikiwa zimetoka Mfuko wa Tume ya Muungano wa Ulaya na milioni 100 zingine kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.
Mkutano huo uliwaleta pamoja takribani washiriki 700 kutoka mashirika ya kimataifa, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na asasi za kiraia.
Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Msataifa Antonio Guterres uliosomwa kwa niaba yake umesema pamoja na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa kutoa dola milioni 24 hapo awali na hata umoja huo kuzindua ombi la msaada wa kibinadamu wa dola milioni 282 ambao umefadhiliwa sehemu ndogo sana, bado mamilioni ya watu wa Msumbiji wanahitaji msaada.
Amesema kuna changamoto kubwa ambapo mahitaji ya msingi ya watu hayafikiwi huku kukiwa na hatari ya kulipuka magonjwa na ukosefu wa chakula kutokana na kupotea kwa mazao wakati wa vimbunga.”
Katibu Mkuu pia ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaongeza juhudi za kushughulikia athari za muda mfupi na za muda mrefu za majanga, na kwamba msaada wa dharua wa kibinadamu sasa utageuka taratibu na kuwa wa ujenzi mpya na kusaidia juhudi za serikali za kuisogeza nchi hiyo katika masuala ya maendeleo.