Pande mbili hasimu nchini Sudan zaanza tena mazungumzo ya ana kwa ana
(last modified Thu, 04 Jul 2019 07:29:19 GMT )
Jul 04, 2019 07:29 UTC
  • Pande mbili hasimu nchini Sudan zaanza tena mazungumzo ya ana kwa ana

Wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko wameanza tena mazungumzo ya moja kwa moja juu ya kipindi cha mpito baada ya kusitiishwa mazungumzo hayo kwa mwezi mzima kufuatia mauaji yaliyofanywa na jeshi la Sudan dhidi ya zaidi ya waandamanaji 100 mbele ya makao ya jeshi mjini Khartoum.

Kikao hicho kilichofanyika jioni ya jana kinahesabiwa kuwa cha kwanza cha ana kwa ana tangu baina ya pande hizo mbili baada ya mauaji ya waandamanaji mjini Khartoum hapo tarehe 3 mwezi uliopita wa Juni na kimehudhuriwa na mpatanishi wa Umoja wa Afrika, Mohamed Hacen El Lebatt na yule wa Ethiopia Mahmud Dirir.

Baada ya masaa kadhaa ya mjadala, pande hizo mbili zimeafiki kuendeleza mazungumzo hii leo Alkhamisi baada ya kukubaliana juu ya udharura wa kuachiwa huru wafungwa wote wa kisiasa.

Mpatanishi wa Ethiopia katika mazungumzo ya amani nchini Sudan, Mahmud Dirir amesema pande mbili zinahitilafiana juu ya idadi ya wawakilishi wa kila upande katika baraza la uongozi la kipindi cha mpito. Vilevile Muungano wa Uhuru na Mabadiliko unataka kuundwe tume huru ya kuchunguza mauaji ya waandamanaji mjini Khartoum.

Jumapili iliyopita, Baraza la Kijeshi la Mpito lilikabiliana kwa mkono wa chuma na maandamano ya wananchi, ambapo watu 11 waliuawa na wengine zaidi ya 180 kujeruhiwa.

Makumi ya waandamanaji wameuawa nchini Sudan

Itakumbukwa kuwa, katika maandamano ya mwezi Mei, zaidi ya raia 118 waliuawa kwa kupigwa risasi na askari usalama mbele ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum. Jeshi la Sudan lilitwaa madaraka ya nchi baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al Bashir mwezi Aprili mwaka huu.

Tags